Isa. 58:7-14 Swahili Union Version (SUV)

7. Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?

8. Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde.

9. Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;

10. na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.

11. Naye BWANA atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.

12. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.

13. Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya BWANA yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe;

14. ndipo utakapojifurahisha katika BWANA; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha BWANA kimenena hayo.

Isa. 58