9. Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.
10. Na wewe, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli; Ninyi mwasema hivi, kwamba, Makosa yetu na dhambi zetu ni juu yetu, nasi tumedhoofika katika dhambi hizo; basi tungewezaje kuwa hai?
11. Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?
12. Na wewe, mwanadamu, waambie wana wa watu wako, Haki yake mwenye haki haitamwokoa, katika siku ya kukosa kwake; na kwa habari ya uovu wake mtu mwovu, hataanguka kwa ajili ya uovu huo, siku ile atakapoghairi na kuuacha uovu wake; wala yeye aliye mwenye haki hataweza kuishi kwa haki yake, siku ile atakapotenda dhambi.
13. Nimwambiapo mwenye haki, ya kwamba hakika ataishi; kama akiitumainia haki yake, akatenda uovu, basi katika matendo yake ya haki, hata mojawapo halitakumbukwa; bali katika uovu wake alioutenda, atakufa katika uovu huo.
14. Tena, nimwambiapo mtu mwovu, Hakika utakufa; kama akighairi, na kuiacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki;
15. kama mtu mwovu akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang’anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa.
16. Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki; hakika ataishi.
17. Walakini wana wa watu wako husema, Njia ya Bwana si sawa; lakini watu hao, njia yao si sawa.
18. Mwenye haki ageukapo, na kuiacha haki yake, na kutenda maovu, atakufa katika maovu hayo.