23. Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake;
24. tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme;
25. ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng’ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote.
26. Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.