1 Sam. 2:31-36 Swahili Union Version (SUV)

31. Angalia, siku zinakuja, nitakapoukata mkono wako, na mkono wa mbari ya baba yako, hata nyumbani mwako hatakuwako mzee.

32. Nawe utalitazama teso la maskani yangu, katika utajiri wote watakaopewa Israeli; wala nyumbani mwako hatakuwako mzee milele.

33. Tena mtu wa kwako, ambaye sitamtenga na madhabahu yangu, atakuwa mtu wa kukupofusha macho, na kukuhuzunisha moyo; tena wazao wote wa nyumba yako watakufa wapatapo kuwa watu wazima.

34. Na hii ndiyo ishara itakayokuwa kwako, itakayowapata wana wako wawili, Hofni na Finehasi; watakufa wote wawili katika siku moja.

35. Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele.

36. Kisha itakuwa, ya kwamba kila mtu atakayesalia katika nyumba yako atakwenda kumsujudia, apate kipande kidogo cha fedha, na mkate mmoja; na kumwambia, Tafadhali unitie katika kazi mojawapo ya ukuhani, nipate kula kipande kidogo cha mkate.

1 Sam. 2