10. na tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi wawe juu ya watu wangu Israeli, nami nitawashinda adui zako wote. Pamoja na hayo nakuambia, ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.
11. Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake.
12. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele.
13. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako;
14. ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.
15. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.
16. Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za BWANA; akasema Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa?
17. Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia sawasawa na hali ya mtu mwenye cheo, Ee BWANA Mungu.
18. Na Daudi akuambie nini tena zaidi kwa habari ya heshima aliyotendewa mtumwa wako? Kwa maana wewe umemjua mtumwa wako.
19. Ee BWANA, kwa ajili ya mtumwa wako, na kwa moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote.